Mkurugenzi Mtendaji wa Malala Fund, Malala Yousafzai
Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi
Shirika la kimataifa la Malala Fund limetenga zaidi ya dola za Marekani milioni 3 kwa ajili ya kuwawezesha wasichana waliokatishwa masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo mimba za utotoni, kurejea shuleni na kuendelea na elimu yao.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Malala Fund, Malala Yousafzai, wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma. Ziara hiyo imelenga kuwatembelea na kuzungumza na baadhi ya wasichana waliopata fursa ya kurejea shule baada ya kukatizwa masomo yao.
Katika mazungumzo yake, Malala amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwawekea vikwazo mabinti waliopata ujauzito kurudi shuleni, akisisitiza kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na njia sahihi ya kutimiza ndoto zao.
“Tumeona Tanzania mabinti wengi wanakatisha masomo kwa sababu ya changamoto mbalimbali, ikiwemo umbali mrefu kwenda shuleni. Malengo yetu ni kushirikiana na taasisi kama Msichana Initiative kutatua changamoto hizi,” alisema Malala.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaondoa watoto shuleni na kuwapeleka kufanya kazi za ndani, akibainisha kuwa hali hiyo inaathiri maendeleo ya elimu na kuongeza mzigo kwa familia na jamii.
“Mtoto akifanya kazi za ndani ni kwa miaka michache tu, baada ya hapo anarudi nyumbani akiwa hana msaada wowote zaidi ya kuwa mzigo. Mbaya zaidi, huko anakumbana na ukatili, magonjwa na mimba zisizotarajiwa,” amesema Mayeka.
Naye Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, ambaye pia ni mdau wa Malala Fund, amesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kuwarejesha shule wasichana takribani 600 waliokuwa wameacha masomo kutokana na sababu mbalimbali kama vile mimba, ndoa za utotoni, umbali wa shule na ajira za ndani.
“Wazazi hupeleka watoto mijini kufanya kazi za ndani kwa matumaini ya kusaidia familia. Lakini kwa waliorejea shule bado kuna changamoto kubwa ya mazingira rafiki, hasa kwa wale wenye watoto,” alisema Gyumi.
Kwa upande wake, Esther Michael, mmoja wa walionufaika na mradi huo, amesema kuwa fursa ya kurejea shule imekuwa kama mwanga mpya katika maisha yake.
Chapisha Maoni