INAWEZEKANA Wakati huu unapitia Wakati
mgumu Sana katika maisha yako na unahisi kukata tamaa, unajiona kama
mtu unayeishi kwenye ukingo wa maisha.
Mambo hayaendi kama
ulivyotarajia. Umekata tamaa. Ukitazama wapi pa kupata msaada, unaona
giza tororo.
Hakuna
tumaini. Ujumbe wangu kwako ni mwepesi. Pamoja na ugumu wa hilo
unalopitia sasa, bado lipo tumaini. Muhimu ni kujua kitu gani unaweza
kufanya unapopita kwenye nyakati ngumu.
Ukweli
ni kwamba hakuna binadamu anayependa shida. Lakini, hata hivyo, shida
hutufundisha mambo ya msingi tunayoyahitaji ili tufanikiwe. Watu wengi
waliofanikiwa, kwa mfano, hawakukwepa shida. Hawakutumia shida zao kama
kisingizio cha kujihurumia na kuwalaumu wengine. Walizichukulia shida
kama mwalimu wa kuwafundisha namna ya kwenda kule wanakotaka kwenda.
Ufanye nini unapopita kwenye nyakati ngumu?
Usijihurumie kupita kiasi
Kuna
mambo ni vigumu kuyakubali yanapotutokea. Kupokea taarifa za msiba,
mathalani, si jambo rahisi. Mara nyingi tunazilazimisha fahamu zetu
zinaamini kinyume chake. Kule kufikiri kuachwa na wapendwa wetu
kunatufanya tuwe kwenye hali ya maombolezo kwa muda mrefu.
Tunaiaminisha
akili kwamba tuko usingizini na kilichotokea ni ndoto tu ya kupita.
Kukana hali ngumu, hata hivyo, huwa ni suluhisho la muda tu.
Kukubali
hali halisi hata kama kufanya hivyo kunakuumiza hisia ni sehemu ya tiba
ya nafsi yako. Kubali uliyempenda amefariki dunia. Kubali kazi
uliyoitegemea haipo tena. Kubali mipango uliyokuwa nayo, haijaenda kama
ulivyopanga. Kubali ndoa uliyofikiri ingekuwa ‘pepo ndogo’ duniani,
haijawezekana. Kubali pengine shauku ya kupata mtoto haitatimia.
Ukikubali kilichotokea bila kujali unajisikiaje, hiyo ni hatua ya kwanza
inayoweza kuanza kubadili maisha yako.
Changamoto
moja wapo inayoweza kukuzuia kukubali hali halisi, ni ile imani kwamba
kilichotokea si haki. Ulichotendewa si haki. Unajiuliza, “Kwa nini
wengine hawapatwi na kile kinachonitokea mimi?” Pambana na mawazo kama
hayo ya kujihurumia. Usipopambana na mawazo kama haya unaweza kuishi na
maumivu kwa muda mrefu sana. Wakati mwingine, unapokuwa kwenye magumu
kama haya jambo muhimu unaloweza kufanya sio kujiuliza kwa nini
kilichotokea kimetokea bali kukubali kwamba ni kweli kimetokea.
Tathmini kile ulichojifunza
Inawezekana
umefukuzwa kazi. Inaumiza kwa sababu hukuwa umejiandaa na mbaya wako
mmoja kazini amekuharibia. Baada ya kukubali kwamba ni kweli sasa huna
kazi, kinachofuata ni kile unachojifunza.
Je,
inawezekana hukujua namna ya kufanya kazi na mtu asiyekupenda? Je,
inawezekana kupoteza kazi ikawa ndio mwanzo wa kufikiri namna ya
kuanzisha na kuendesha shughuli zako mwenyewe?
Siku zote kuna upande mzuri kwenye kila kibaya kinachokutokea. Jitahidi kuufahamu upande huo.
Nawafahamu
watu wengi waliolazimika kufungua biashara zao na wakapata mafanikio
kwa sababu tu walifukuzwa kazi. Wasingefanyiwa fitna kazini na kupoteza
kazi, wangeendelea kuajiriwa kwa muda mrefu ujao. Kumbe nyakati ngumu
kama hizi ukizitumia vizuri zinaweza kukufungua macho na kubadilisha
kabisa uelekeo wa maisha yako.
Pengine
ni madeni. Je, umejiuliza kwanini kila mtu anakudai na unapata
mshahara unaowatosha watu wengine? Je, kuna namna ambayo ungeweza
kukwepa madeni hayo kama ungejifunza jambo fulani? Je, inawezekana ni
mtindo wako wa maisha umechangia kuingia kwenye matatizo yasiyo ya
lazima? Pamoja na ubaya wa madeni, wakati mwingine, unaweza kuingia
kwenye tatizo la kudaiwa, ili uone matokeo ya kufanya maamuzi ya kifedha
yasiyo sahihi. Kudaiwa kunaweza kuwa fursa ya kubadilika.
Usijitenge na watu
Ni
kweli, wakati mwingine, kujitenga kunaweza kukusaidia kuwaepuka watu
wanaoweza kukufanya ukajisikia vibaya zaidi. Hata hivyo, ukaribu na
watu wanaoaminika ni hatua muhimu kuchukua unapopita katika kipindi
kigumu. Watu wenye mtazamo chanya, kwa mfano, ndio watakaokusaidia
kukutia moyo, kukufariji na kukutazamisha mambo kwa namna
itakayochangamsha tena moyo wako.
Kwa
vyovyote vile unawafahamu watu katika maisha yako unaoweza kusema
unawaamini. Hawa ni watu mnaoaminiana na kuheshimiana. Hawa si watu
wepesi kukushambulia, kukuhukumu na kukuonyesha namna gani hali Hali
uliyonayo hukupaswa kuwa nayo.Jitahidi kupambana nayo.
Tafuta msaada zaidi
Unahitaji
msaada wa mawazo. Mahali pa kuanzia watu ulionao karibu kupitia vikundi
vya kijamii ulivyonayo tayari mfano kanisani au msikitini. Hata kama
huwafahamu zaidi watu hawa kiundani, bado kwa kule kuwa nao karibu
itakusaidia kuyatazama maisha kwa sura ya matumaini. Kaa karibu na
vikundi hivi ujijenge kiimani. Nyakati ngumu ziwe kichocheo cha kuwa
karibu na Muumba wako.
Lakini
pia, ni vizuri wakati mwingine kukutana na watu waliowahi kupitia
changamoto yako wanaoweza kukupa mawazo chanya ya namna ya kukabiliana
nayo. Kama umepoteza kazi, mathalani, na kuna mtu unayemfahamu aliwahi
kupoteza kazi pengine unahitaji kuonana naye kupata uzoefu wa namna
alivyoweza kupita kipindi hicho.
NB: Kaa karibu na Mungu zaidi na atakusaidia usijiingize katika mambo mabaya Kwa kigezo cha kuondoa mawazo utapotea!
Chapisha Maoni